Mnamo Tarehe 17 Machi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alitangaza kufungwa kwa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Machi 17 kama njia ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa korona, maarufu kama COVID-19. Tarehe 14 Aprili Waziri Mkuu alisema agizo la kufungwa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vyote vya elimu ya kati na vya elimu ya juu, litaendelea kubaki vile vile hadi hapo serikali itakapotoa tamko lingine.

Kutokana na hatua hizi muhimu ambazo serikali imeendelea kuchukua ili kupunguza kusambaa kwa maambukizi katika nchi yetu, baadhi ya jamii zetu zimekuwa zinatumia mwanya huu kuendeleza vitendo vya ukeketaji na kuwaozesha watoto wa kike, kwa sababu tu hawako katika mfumo wa shule unaoweza kutoa ulinzi na ufuatiliaji dhidi ya vitendo hivi vya ukatili.
Kama mashirika tunayotetea haki na ulinzi wa mtoto wa kike, tunalaani vitendo hivi, jamii, wazazi na wale wote wanaotumia muda huu kufanya na kuendeleza vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni kwa wasichana badala ya kuchukua jukumu la malezi na ulinzi kwa watoto wakati huu wakiwa nyumbani.

MATUKIO YALIYOTOKEA/KURIPOTIWA
Katika wilaya ya Tarime, jumla ya watoto 557 walikimbilia katika kituo cha Masanga baada ya kulazimishwa kukeketwa na jamii zao mwaka 2019. Baada ya msimu wa ukeketaji kuisha jumla ya watoto 451 walirudishwa majumbani kwao baada ya kufanya majadiliano na wazazi wao na wakaridhia kuwapokea, lakini watoto 106 walikataliwa na wazazi wao hivyo kulazimika kubaki kituoni.
Baada ya shule kufunga kwa sababu ya janga la korona watoto hao walirudi katika familia zao, ndipo wazazi wamechukua kama fursa kwao na kuendelea kuwakeketa watoto. Jumla ya matukio 17 yameripotiwa katika kituo cha Masanga ya watoto waliokeketwa baada ya shule kufunga, takribani wasichana 160 walifanikiwa kutoroka na kurudi kituoni Masanga ili kupata hifadhi, hata hivyo watoto wengi wamekeketwa na zoezi la ukeketaji linaendelea mpaka sasa.
Wilayani Serengeti kupitia shirika la Hope for Women and Girls Jumla ya wasichana 33 wameokolewa kwa kipindi cha April 1 hadi 15. Wasichana 6 walikutwa wamekeketwa na familia 6 zimekamatwa na kesi zimepelekwa mahakamani.
Katika eneo la Loliondo zaidi ya wasichana 10 wamepigwa na wazazi wao wakilazimishwa kuolewa katika kipindi hiki cha shule kufungwa. Kupitia mashirika yetu tumekuwa tunapokea wasichana waliokimbia kukeketwa wakitafuta sehemu salama ya kujihifadhi dhihi ya ukatili huu. Pia wasichana waliokimbia kuozwa kwa lazima na wazazi wao katika umri mdogo.

HALI YA UKEKETAJI NA NDOA ZA UTOTONI
Kwa mujibu wa utafiti wa Takwimu za Demografia na Afya (TDHS) wa mwaka 2015/16 inaonesha tatizo la ukeketaji lipo kwa asilimia 10 katika nchi yetu kutoka asilimia 18 iliyorekodiwa mwaka 1996 miaka michache kabla ukeketaji haujapitishwa kuwa kosa la jinai kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu, 1998.
Ieleweke kuwa Ukeketaji ni kinyume na sheria na kitendo kinachomdhalilisha mtoto wa kike na kumwondolea utu wake kama mwanadamu aliyeumbwa kamili. Ukeketaji mara zote hufanyika kwa sababu ya misukumo ya kibinadamu, ikiwemo kupata mali kwa kumwozesha binti aliyekeketwa, kutii
masharti ya mila kama ya kutambika mizimu, kuondoa mikosi katika familia, kumvusha mtoto rika na nyinginezo nyingi. Hata hivyo sababu hizo zote hazina maana zaidi ya kuendeleza tamaduni kandamizi kwa wanawake na watoto wa kike.
Kwa upande wa ndoa za utotoni, wasichana wawili (2) kati ya watano (5) huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 (TDHS 2015/16). Mwaka 2016 Serikali kupitia Bunge lilibadili Sheria ya Elimu, 1978 na kuweka kuwa kosa kwa mtu yeyote atakayemuoa au kumpa mimba mwanafunzi. Mwaka 2019 kupitia Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Mahakama ilitamka kuwa umri wa chini wa kuoa na kuolewa utakuwa ni miaka 18 kwa wasichana wavulana.
SHERIA, SERA NA MIPANGO INAYOPINGA UKATILI KWA MSICHANA
Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa yenye lengo la kuboresha hali za wasichana, ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (CRC) wa mwaka 1989 na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa mwaka 1990. Kwa hapa nchini tuna Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo inataja haki za msingi za mtoto kama zilivyoelezewa kwenye mikataba hiyo na kueleza wazi kwamba katika kufanya maamuzi yoyote kuhusu mtoto kanuni ya maslahi mapana ya mtoto lazıma izingatiwe.
Mikataba hii na sheria ya mtoto inatoa wajibu kwa serikali, wazazi, walezi na wanajamii kwa ujumla kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili na ubaguzi. Serikali ina sera na mipango mbalimbali yenye lengo la kumlinda mtoto wa kike na kumaliza ukatili ikiwemo Mpango Kazi wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto ( MTAKUWWA 2017/18 – 2019/2022) ambao umelenga kwenye kuongeza ulinzi na kuzuia unyanyasaji kwa mtoto wa kike.
Pamoja na jitihada hizii, bado wasichana wameendelea kuwa wahanga wa aina mbalimbali za ukatili, hasa ukatili wa kingono.

WITO WETU
Mpaka kufikia March 23, zaidi ya nchi 138 ikiwemo Tanzania zilikuwa zimefunga mifumo yao ya elimu kutoka na mlipuko wa ugonjwa wa korona. Hatua hizi zimechukuliwa ili kudhibiti maambukizi. Kutokana na shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO zaidi ya aslimia 80 ya wanafunzi duniani wameathirika kutokana na hatua hizi.
Tunawasiwasi wa kuongezeka kwa vitendo vya ukatili kwa watoto ikiwemo ubakaji, ulawiti, vipigo, matusi wakati huu watoto wapo nyumbani. Asilimia kubwa ya vitendo vya ukatili kwa watoto hufanyika nyumbani na kuhusisha watu wa karibu wakiwemo wazazi, ndugu na majirani.
Tanzania ni nchi ya 10 kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wenye umri mdogo. Vijana balehe ni asilimia 32 ya watu wote (sensa 2012). Ni muhimu kuwa na jitihada zenye lengo la kuhakikisha kundi hili kubwa linalindwa na kubaki salama hasa katika kipindi hiki ambacho nguvu kubwa ipo kwenye kukabiliana na janga la korona.
Kama mashirika tunayofanya kazi kwenye masuala ya ulinzi wa mtoto, tunapendekeza mambo yafuatayo ili kunusuru hali inayoendelea na kuwalinda watoto na athari kubwa zaidi zinazoweza kuwapata kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatili

1. Serikali kupitia uongozi wa serikali za Mtaa na vijiji kuweka mkakati maalum wa makusudi kabisa wa kuwalinda watoto wote nchi nzima dhidi ya matukio ya ukatili na udhalilishaji hasa ukeketaji,ndoa za utotoni, ubakaji, ulawiti na mengine mengi katika kipindi hiki cha ugonjwa wa korona.
2. Tunasisitiza jamii,wasichana na watoto kwa ujumla kuripoti matukio yote yenye viashiria vya ukatili kupitia namba 116 ambayo ni namba maalum kwa ajili ya kuripoti matukio ya ukatili na udhalilishaji dhidi ya watoto inayopatikana saa 24 siku zote, ili waweze kupata msaada wa haraka.
3. Serikali kwa kupitia vyombo vyake kusimamia sheria, kanuni na taratibu hasa kwa wanajamii wote watakaobainika kufanya vitendo vya ukeketaji na kuozesha watoto kwani ni kinyume na sheria za nchi.
4. Tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, viongozi wa kisiasa waache kutoa kauli za kuhamasisha vitendo hivi ili kujipatia umaarufu na kura kutoka kwa wananchi
5. Wazazi kuwa mstari wa mbele katika kuwalinda watoto hasa watoto wa kike dhidi ya ukatili unaowalenga wao katika kipindi hiki.
6. Wachochezi wa Ukeketaji – wazee wa mila na ngariba walioshiriki kukeketa wachukuliwe hatua kali wachukuliwe hatua kali ili iwe mfano kwa wote watakaotaka kuvunja sheria za nchi kwa kudhalilisha watoto wa kike.
7. Serikali itilie mkazo tohara salama kwa vijana, – tohara zifanyikie hospitali ili kupunguza idadi ya vijana wanaohitaji kuoa wanawake waliokeketwa, hii itatoa fursa kwa vijana kupata elimu ya madhara ya ukeketaji na madhara ya kuoa mwanamke aliye keketwa.
8. Jamii kutoa ushirikiano katika kusimamia sheria, kanuni na taratibu pale watakapohitajika hasa kutoa ushahidi mahakamani katika kesi zinazohusu ukeketaji na ndoa za utotoni.

IMETOLEWA NA MASHIRIKA YAFUATAYO LEO TAREHE 16 Machi 2020:

1. ATFGM – MASANGA
2. MSICHANA INITIATIVE
3. C-SEMA
4. MIMUTIE WOMEN ORGANISATION (MWO) – LOLIONDO
5. CHILDREN’s DIGNITY FORUM (CDF)
6. HOPE FOR WOMEN AND GIRLS IN TANZANIA